Kuwa na mafanikio
makubwa na unayoyataka katika maisha yako ni kitu cha muhimu sana. Na ili uwe
na mafanikio hayo, kuna umuhimu mkubwa wa wewe kubadili namna unavyoishi sasa.
Kama utaendelea kuishi maisha unayoishi hivi sasa na huku ukiwa unataka
mafanikio makubwa yatokee kwako ni kitu ambacho hakitawezekana.
Ili uweze kusonga mbele
na kufanikiwa, kuna vitu ambavyo utalazimika kuvibadili au kuachana navyo
kabisa katika maisha yako. Kama hautachukua hatua ya kuachana na vitu hivi
mapema uwe na uhakika utaendelea kuishi maisha yaleyale siku zote. Na kati ya
mambo unayotakiwa kubadili na kuachana nayo ni kuacha kuogopa sana maisha.
Umefika wakati wa
kutenda bila kuogopa chochote na achana na mambo yanayokukwamisha na kukuzuia
kufikia kwenye kilele cha mafanikio. Maisha hayakusubiri wewe kama huchukui
hatua mapema yanazidi kusonga mbele na miaka inakatika tu. Ukijichunguza kwa
makini utagundua kuwa vipo vitu vingi ambavyo umekuwa ukiviogopa na vimekuwa
kizuizi kikubwa cha wewe kufanikiwa.
Kumbuka dunia
tuliyonayo sasa imesonga mbele sana,
kwa nini ukubali kusimama palepale
ulipokuwa miaka kumi nyuma. Huna haja ya kuogopa na kuamini tena
wengine ndio wanaoweza
kufanikiwa, sasa ni zamu
yako ya kuishi maisha ya mafanikio. Kama
kweli unataka mafanikio makubwa katika maisha yako, acha kuogopa kufanya mambo
haya tena:-
1. Acha
kuogopa kujitoa mhanga.
Kama unataka ndoto zako
zitimie na kufanikisha malengo makubwa unayoyataka ni lazima ujifunze kujitoa
mhanga juu ya ndoto zako. Watu wengi huwa wanapenda mafanikio makubwa yawe kwao,
lakini huwa hawajali suala hili sana la kujitoa mhanga. Bila kujitoa mhanga
itakuwa ni ngumu sana kutimiza baadhi ya ndoto zako.
Kuna wakati katika
kufanikisha malengo yetu kiuhalisia mambo huwa yanakuwa magumu na wengi
hujikuta wakiacha ndoto zao zikipotea. Kitu pekee ambacho kitakuokoa na
kukufanikisha ni kujitoa mhanga. Ni kweli unaona mambo magumu sana, lakini hakuna kukata tamaa.
Pigana mpaka tone la mwisho, jilipue kwenye ndoto zako, mwisho utafanikiwa .
Watu wengi wenye
mafanikio makubwa duniani walijitoa kwenye ndoto zao hadi zikafanikiwa. Acha
kuogopa kujitoa mhanga juu ya ndoto zako na kisikutishe kitu chochote unaweza.
Kama ni shida ulizonazo ni za muda tu. Mbele yako yapo mafanikio makubwa sana
usiyoyajua. Mafanikio hayo utayapata kama tu, kama utaamua kung’ang’ania ndoto
zako bila kuacha.
2. Acha
kuogopa kujiwekea malengo makubwa.
Haijalishi unaishi
wapi, huna pesa au ni maskini kiasi gani lakini kitu muhimu unachotakiwa kuwa
nacho ni lazima uwe na ndoto kubwa. Wapo watu ambao huwa wanaogopa kuwa na
ndoto kubwa maishani mwao eti ni kwa sababu hawana pesa. Ni watu ambao
wanasubiri wawe na pesa za kutosha ndio wawe na ndoto kubwa.
Kujiwekea malengo
makubwa katika maisha yako ni kitu ambacho haulipii. Kama ndoto hazilipiwi ni
nini kinachokuzuia kuota ndoto kubwa? Hata kama unalala darajani hauzuiliwi na
mtu wala polisi hawataweza kukukamata eti kwa kuwaza kwamba, lazima siku moja
uje umiliki Hotel kubwa kama Kilimanjaro
Hotel. Kikubwa uwe na mipango na malengo utafika.
3. Acha
kuogopa sana matatizo uliyopitia.
Inawezekana kabisa kuna
sehemu uliumizwa katika maisha yako sasa unaogopa tena kusonga mbele. Kama upo
katika hali hii isikukatishe tamaa, acha kuumia kwa sababu ya hasara pengine
uliyoipata wala acha kusimama endeleza ndoto zako. Maumivu uliyonayo sasa hivi
yasikuzuie kuendeleza ndoto zako hata kidogo.
Kumbuka maumivu ni
sehemu ya kukua na sehemu ya kujifunza pia katika maisha yetu. Kama kuna sehemu
ulikosea katika mradi wako acha ile tabia ya kitoto ya kuzira na kusema sitaki
tena kusikia habari hiyo, unataka mafanikio makubwa katika maisha yako, acha
kuogopa sana matatizo.( Unaweza ukasoma pia Vitu Muhimu Unavyotakiwa kukumbuka Wakati Mambo Yako Yanapokwenda Hovyo.
4. Acha
kuogopa kuishi maisha ya mafanikio unayoyataka.
Asije akakuzuia mtu kwa
kukuambia huwezi kufanikiwa kwa malengo uliyojiwekea. Wapo watu ambao katika
maisha yetu huwa ni wepesi sana kukatisha tamaa wenzao. Kwa kulijua hilo ni
muhimu sana kuwa nao makini, maana wasije wakakufanya ukaachana na ndoto zako
na ukawa mtu wa kuogopa kuishi maisha ya mafanikio unayoyataka.
Jifunze kuishi kwa
malengo uliyojiwekea, fuata ndoto zako na pia kuwa dereva wa maisha yako mwenyewe kwa kuishi maisha ya mafanikio unayoyataka. Achana na watu watakao taka kukupangia maisha yako ya
mafanikio. Kumbuka kila mtu hapa duniani amekuja na malengo yake, acha
kuyumbushwa, simama imara na tekeleza mipango yako kikamilifu.
5. Acha
kuogopa kufanya mabadiliko.
Kati ya vitu vigumu
katika maisha ya mwanadamu ni kufanya mabadiliko. Hata kama ipo wazi kabisa
kwamba mabadiliko hayo yataleta faida kwake bado pia huwa ni ngumu kubadilika.
Hii yote inaonyesha ni jinsi gani sisi tukiwa kama binadamu, ni tulivyokuwa
wagumu kubadilika.
Kwa hiyo hapo utaona
kabisa kufanya mabadiliko katika maisha yako inahitajika ujasiri, ili uweze
kushinda hilo na kufanikiwa kusonga mbele. Kama nilivosema wakati naanza makala
hii ni lazima kubadili baadhi ya tabia zetu mbaya ili tufanikiwe. Acha
kuziogopa kuzifanyia mabadiliko tabia zinazokukwamisha kufanikiwa.
6. Acha
kuogopa kujifunza kutokana na makosa.
Ni kweli kuna sehemu
umekosea katika maisha yako, lakini kila unapokumbuka inakuuma sana na mpaka
unashindwa kujifunza kutokana na makosa uliyoyafanya. Ninachotaka kukwambia
acha kuogopa kujifunza kutokana na makosa ambayo yameshafanyika na isitoshe
yamepita.