CHUO Kikuu Ardhi (ARU), kimewazawadia wanafuzi 130 wa masomo mbalimbali zawadi zenye thamani ya zaidi ya sh milioni 60 kutokana na ufaulu mzuri katika masomo yao.
Zawadi hizo ni fedha taslimu, mashine za upimaji ardhi na ‘laptop’ katika hafla fupi iliyofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam juzi.
Akikabidhi zawadi hizo, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Idrissa Mshoro, alisema kuwa wanafunzi wa kike wameendelea kufanya vizuri katika masomo yao, ambako wamefikia wastani wa asilimia 40 dhidi ya 30 za wanaume.
Alisema miongoni mwa wanafunzi waliopata zawadi hizo, hawakuwa na sifa za kujiunga katika chuo hicho mpaka walipopewa kozi fupi ambapo baada ya usaili walifaulu.
Prof. Mshoro, alisema kuwa waliamua kuwa na mfumo huo baada ya kuona wanafunzi wengi wanataka kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya elimu ya juu lakini alama zao walizopata katika shule walizokuwa wanasoma haziwawezesha kujiunga.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Taaluma chuoni hapo, Gabriel Kassenga, alisema kuwa matokeo ya mwaka huu yameendelea kufuta dhana kuwa wanawake sio wazuri katika masomo ya sayansi.