WAKATI Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ikielezwa kuwa taratibu za mazishi ya mtuhumiwa wa pili katika kesi ya ugaidi ya tukio la mlipuko wa bomu katika Baa ya Arusha Night Park, Ustadhi Abdulkarim Thabit, zinaendelea, imefahamika kuwa mtuhumiwa huyo alishazikwa tangu Desemba 2 mwaka huu.
Mmoja wa Askari Magereza ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, jana aliieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Hawa Mguruta, kuwa mtuhumiwa huyo alifariki Desemba Mosi mwaka huu, kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru alipokuwa amelazwa tangu akamatwe na taratibu za mazishi zinaendelea.
Kesi hiyo na nyingine 13 ambazo zimepangwa kutajwa siku moja katika Mahakama hiyo, ziliahirishwa hadi Desemba 19 mwaka huu, kutokana na upelelezi wake kutokamilika.
Aidha, watuhumiwa hao walipoanza kuitwa majina yao, askari huyo aliieleza Mahakma kuwa, Thabit amefariki dunia na mazishi yanashughulikiwa.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Agustino Kombe, aliieleza Mahakama hiyo kuwa, upande wa Jamhuri haukuwa na taarifa hizo ambako wakipata taarifa hiyo kutoka Magereza wataleta maombi mahakamani hapo kubadili hati ya mashitaka ili wamuondoe mshtakiwa huyo aliyefariki.
Kwa upande wake, Ustaadhi wa msikiti wa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Shaaban Salum, alisema alipata taarifa za kufariki kwa Ustadhi Thabit Desemba 2 mwaka huu majira ya saa 1:00 asubuhi.
Alisema kuwa, kipindi chote alichokuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo, alikuwa akimnunulia dawa za kumsafisha vidonda alizokuwa akiagizwa na manesi na madaktari waliokuwa wakimuhudumia, lakini hakuwahi kumuona kwani alikuwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza.
“Mimi Askari Magereza alinifuata pale msikitini akaniambia Ustaadhi Thabit alifariki jana (Desemba 1, mwaka huu) majira ya saa 11 jioni, kwenye saa 2:30 asubuhi, wakaja ndugu zake tukaenda chumba cha kuhifadhia maiti…
“Tulimkuta ana vidonda mgongoni na kwenye makalio… tulipotoka pale tukaenda kuandaa mazishi. Tulimzika siku hiyohiyo kwenye makaburi ya Waislamu Njiro,” alisema Ustaadhi Salum.
Katika kesi hiyo, marehemu Ustadhi Thabit, anadaiwa yeye na washtakiwa wenzake, wanadaiwa kufanya uwakala na kusajili vijana kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab cha nchini Somalia.
Wanadaiwa kuhusika na tukio la ugaidi la kurusha bomu katika baa ya Arusha Night Park iliyopo jijini hapa na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 15, Aprili 14 Mwaka huu.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo tangu akamatwe hakuweza kufika mahakamani,ambako alilazwa katika hospitali hiyo na kusomewa mashitaka akiwa wodini.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Dk. Josian Mlaya, alithibitisha kuwa Ustaadhi Thabit alifariki Desemba Mosi mwaka huu, ingawa hakuwa tayari kuingia kwa undani juu ya chanzo cha kifo hicho.