MKUU wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Evarista Kalalu, amewashauri wananchi wa vijiji vya Ukami na Chogo Kata ya Mapanda wilayani hapa na viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo wenyeviti wa vitongoji, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ikiwa ni njia ya kuondokana na gharama za matibabu kipindi hawana fedha.
Kalalu, aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye siku ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo, ili kujihakikishia matibabu stahiki kupindi chote hata kile ambacho watakuwa hawana fedha.
Alisema kaya nyingi zinashindwa kupata matibabu pindi wanapokosa fedha, kwa kushindwa kufahamu umuhimu wa mfuko wa jamii na kujiunga nao na kuwataka kujiunga nao kwani una faida nyingi kwa wananchi wa kipato cha chini pindi wanapokosa fedha za matibabu.
“Uelimishaji unahitajika kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, Kata na Tarafa kwa kufanya mikutano ya kuhamasisha na uelimishaji. Pia wenyeviti wa vitongoji, watendaji na wengineo ambao bado hawajajiunga na mfuko huu, muonyeshe mfano kwa kujiunga na kuweza kuwashawishi wananchi waliowengi katika vijiji mnavyoishi kujiunga katika Mfuko wa Afya ya Jamii kwa lengo la kuondokana na gharama nyingi zaidi,” alisema.
Aidha, Kalalu alizitaja faida za mfuko huo kuwa ni mwananchi kupata huduma ya matibabu wakati wote hata kama hana fedha na mfuko utatoa uhakika wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba mwaka mzima kwa kuchangia sh 5,000 kwa mwaka.
Awali, Meneja wa CHF Mkoa wa Iringa, Emmanuel Mkwabi, alisema kuwa mfuko huo ni mkombozi halisi wa Mtanzania wa kipato cha chini, kwa kuwa ni ukweli usiopingika kwamba ugonjwa hautoi taarifa, hauchagui siku wala mtu, hivyo upo uwezekano mkubwa kumpata mtu akiwa hana fedha kabisa.