ameshinda rufaa ya maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na Serikali kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kumfutia mashitaka ya ugaidi.
Lwakatare, alipata ushindi huo jijini Dar es Salaam jana katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, baada ya kutupilia mbali maombi ya Jamhuri ambayo yalilenga kupinga uamuzi uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri Mei 8, 2013.
Lwakatare alikuwa akitetewa na Mawakili Peter Kibatala akisaidiana na John Malya huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Faraja Nchimbi.
Akisoma uamuzi huo, Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Zahara Maluma, alisema rufaa ya Jamhuri haikuambatanishwa na kumbukumbu za Mahakama Kuu katika uamuzi wa Jaji Kaduri, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Alisema katika maelezo ya rufaa aliyoyasoma mbele ya Mawakili wa pande zote mbili, hakuna sehemu iliyoambatanishwa kumbukumbu ambazo zinaonyesha marejeo kuhusu uamuzi huo uliopita.
Baada ya kutolewa uamuzi huo, Wakili Kibatala alisema kwamba, Mahakama hiyo inapaswa kupongezwa kutokana na kutenda haki bila ya kuangalia upande wowote.
“Naamini kama maamuzi yatakuwa hivi katika kesi zote, tutazidi kuimarisha imani ya mawakili kutokana na hukumu zinazotolewa katika kesi mbalimbali,”alisema.
Kufutwa kwa shauri hilo, kunatokana na ombi lililowahi kuwasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi wakati huo, kuiomba mahakama hiyo itengue uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wa kumfutia mashitaka matatu ya ugaidi Lwakatare.