MWENYEKITI wa Kamati ya Maandalizi siku ya Usafiri wa Anga, Mtesigwa Maugo amesema wamewawezesha wanafunzi 20 kutoka shule tofauti za msingi jijini hapa kwenda Zanzibar kutembea wakati wa maadhimisho ya siku hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima kwenye maonesho ya wiki ya usafiri wa anga inayofikia kilele chake Desemba 7, Maugo alisema wanafunzi hao waliondoka kwa ndege ya kukodi yenye namba za usajili 5H-TGF.
Alisema safari hiyo inalenga kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi yatakayowasaidia kuingia katika utaalam wa masuala ya usafiri wa anga.
“Nimefurahi kuona watoto wa kike wengi wanafanya vizuri katika masomo ya sayansi nao wapo kwenye safari hiyo,” alisisitiza Maugo.
Alitaja shule za msingi walizotoka wanafunzi hao kuwa ni Tungi iliyopo Kigamboni, Juhudi iliyopo Ilala na kituo cha kulea yatima kilichopo Kinondoni huku akisisitiza kwamba uchaguzi wao umegusa wilaya zote tatu za jiji hili.