Waandamanaji wameingia katika barabara za miji mingi Nchini Marekani kwa usiku wa pili mtawalia, kupinga maamuzi ya majaji kutupilia mbali kesi dhidi ya afisa wa polisi aliyedaiwa kumuua raia mmarekani mweusi nchini humo Eric Garner.
Mjini New York, waandamanaji wameonekana wakibeaba kaburi bandia wakivuka daraja la Brooklyn Bridge huku wakitatiza msongamano wa magari barabarani mjini New York.
Meya wa jiji hilo, Bill de Blasio, amewaambia wanahabari kuwa uhusiano kati ya maofisa wa polisi na raia wa Marekani, unafaa kubadilika, na watu wanafaa kufahamu kuwa maisha ya watu weusi ni sawa na ya watu weupe.
Mnamo Jumatano, Polisi jijini New York waliwatia mbaroni watu 83 baada ya maandamano mengine kutokea siku ambayo maandamano hayo yalianza baada ya mahakama kutupilia mbali kesi dhidi ya askari mzungu kwa kumuua Eric Garner.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wameweka matumaini yao katika maafisa wa polisi watakaoufanyia kesi hio uchunguzi zaidi.
Meya wa New York, Bill de Blasio, amenukuliwa akisema kuwa polisi 22,000 walioko mjini humo watapewa mafunzo zaidi kuhusu namna ya wanavyowakamata wahalifu au washukiwa wa uhalifu.
Rais Barack Obama amesifu tamko la Meya akisema kuwa wamarekani wengine wanahisi kutokuwepo usawa katika sheria na ambavyo inatekelezwa.