Msaidizi wa kazi za ndani (hausigeli), Rehema Ally (17), mkazi wa
Yombo, Machimbo Mwisho, Ilala jijini Dar, amechanwachanwa kwa wembe na
kisu sehemu mbalimbali za mwili wake, hali iliyosababisha alazwe katika
Hospitali ya Amana kwa matibabu.
Rehema Ally akiwa na majeraha mwilini mwake baada ya kujeruhiwa.
Akizungumza na Uwazi nyumbani kwa mwajiri wake aliyejulikana kwa jina
moja la Ghati, Yombo jijini Dar, Rehema aliyefika jijini hapa Januari,
2013 akitokea nyumbani kwao, Masasi mkoani Mtwara, alikuwa na haya ya
kusema:
“Nakumbuka siku hiyo ilikuwa ni Jumapili ya Novemba 30, saa moja
usiku nikiwa nje ya nyumba ya bosi wangu. Akatokea msichana mmoja
aitwaye Fatuma na mwenzake aitwaye Ashura huku wakiwa wamebeba kisu na
wembe. Wakanikamata kwa nguvu na kunikaba, wakaniangusha chini na kuanza
kunichanachana mwili mzima.
“Wakati huo nilikuwa naelekea nyumbani kwa akina Fatuma kuchukua
sanduku langu ambalo alilichukua kwa bosi wangu akidai kwamba
nimempotezea ‘memori kadi’ ya simu yake hivyo alisema kwamba mpaka
nitakapomrudishia ndipo nitakapochukua sanduku langu.
“Walinijeruhi sana na kukimbia, nikarudi ndani lakini bosi wangu
hakuwepo nyumbani na aliporudi alinichukua na kunipeleka polisi,
tukapewa kibali cha matibabu (PF3) na kwenda Hospitali ya Amana
kutibiwa. Tulirudi nyumbani na baadaye tukafuatilia kesi yetu polisi,
wakasema turudi nyumbani tukaelewane mbele ya mjumbe ili kesi imalizike.
“Tulienda kwa mjumbe pamoja na Fatuma na wazazi wake na mimi nilikuwa
na bosi wangu, wakataka kesi imalizike yaani tusameheane lakini kwa
upande wa wazazi wangu waliopo Masasi, nilipowapa taarifa walikataa
kumaliza kesi kienyeji na kutaka ifike mahakamani kwa vile watuhumiwa
walikuja na silaha na walidhamiria kuniua,” alisema Rehema.
Kwa upande wa mtuhumiwa, Fatuma Zuberi (17), alipoulizwa na waandishi
wetu, alidai kwamba wakiwa njiani na mdogo wake wakienda dukani kununua
vocha, walivamiwa na Rehema na kushambuliwa akitaka wamrudishie sanduku
lake.
Naye mama mzazi wa Fatuma aliyejitambulisha kwa jina la Sharifa
Mwinyi Kondo, alidai kwamba mwanaye pia amejeruhiwa hivyo waliamua mambo
yote yaishe kwa kusameheana mbele ya mjumbe wao. Mjumbe wa shina namba
22, Rose Kiravu alipoulizwa kuhusu ishu hiyo alikiri kupokea taarifa
hizo na kudai kwamba suala hilo lilifika polisi lakini lilirudishwa
kwake kwa upatanishi ambapo alikaa na pande zote mbili pia wajumbe wa
nyumba kumi wawili na wote waliamua kusameheana.