BARAZA la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), limeitaka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa (Tamisemi), kutoa majibu ya haraka juu ya kuenguliwa kwa wagombea wa chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BAVICHA, Julius Mwita, alisema kuwa wagombea wa chama chao wameenguliwa katika kinyang’anyiro hicho kwa sababu zisizokuwa za kimsingi.
Alifafanua kuwa, hizo ni mbinu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kutumia viongozi walioko madarakani kutaka kuwapitisha wagombea wao ili kuwasaidia katika uchaguzi mkuu ujao.
“BAVICHA hatuko tayari kuona uonevu wa kiasi hiki tunaufumbia macho, tunamtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa majibu ya haraka kuhusiana na hili kabla ya siku ya uchaguzi,” alisema Mwita.
Alitaja baadhi ya maeneo aliyopata taarifa kuwa Kamati ya Rufaa imewaengua wagombea wao ni Same, Vunjo, Njombe, Simanjiro na Mwanza.
Aliongeza kuwa, kuna baadhi ya maeneo ambayo wabunge wa CCM wanawalazimisha wakurugenzi wawaengue wagombea wa CHADEMA.
Akizungumzia miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika, Mwita aliwataka vijana kuadhimisha kwa kutafakari hali yao kimaisha, kwani Watanzania walio wengi bado ni masikini, hivyo ni wakati wa kufanya mabadiliko kuanzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Kesho ni sikukuu ya uhuru wa Tanganyika, ni wakati muafaka wa kuangalia je ndani ya miaka 53 tumeweza kupigana na adui umasikini, ujinga na maradhi huku jingine limeongezeka rushwa, hivyo basi ni wakati muafaka kwa Watanzania kufanya mabadiliko kuanzia ngazi ya kata,” alisema.