Serikali ya Tanzania iko hatarini kukosa dola za Marekani milioni mia
saba sawa na trilioni 1.1 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya mradi wa
pili wa mfuko wa changamoto za Milenia (MCC) kutokana na kushamiri kwa
vitendo vya rushwa nchini humo.
Haya yanajiri wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa kutoa maamuzi ya
mapendekezo yaliyofikiwa na Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji fedha
zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kaunti ya Tegeta Escrow wiki ijayo.
Marekani imebainisha kuwa mkataba wa pili wa miradi inayofadhiliwa na
shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) utategemea hatua
zitakazochukuliwa na serikali ya Tanzania dhidi ya wahusika wa kashfa
hiyo.
Katika tamko hilo kwa umma ambalo limewekwa kwenye tovuti ya MCC,
bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu
wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania Desemba 9, mwaka huu kwamba
itachukua hatua za haraka na kutoa maamuzi dhahiri na thabiti kuhusu
maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL.
Taarifa iliyotolewa na
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ilieleza kuwa wakurugenzi wa MCC
waliokutana katika mkutano wao uliofanyika Desemba 10, mwaka huu
wamesikitishwa na hali ya rushwa nchini Tanzania.
Uamuzi huo wa Marekani ambayo inafadhili miradi mingi ya mabilioni ya
fedha ni mtihani wa pili kwa Rais Kikwete baada ya ule wa maazimio ya
Bunge yaliyotaka viongozi wakiwamo mawaziri waliotajwa katika kashfa
hiyo kuwajibishwa.
Wanaotakiwa kuwajibishwa na Rais Kikwete ni
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo na Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Novemba
mwaka huu, Serikali ya Marekani kwa kupitia MCC, ilikubali kutoa ruzuku
ya hadi Dola za Kimarekani milioni 9.78 kwa ajili ya maandalizi ya
miradi ya uwekezaji yenye matokeo makubwa katika sekta ya nishati
nchini.
Tanzania ilikuwa mojawapo ya nchi kumi zilizojadiliwa na
Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizo zimekidhi vigezo vya
kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya.
Wakati wa mkutano
wa 16 na 17 wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
(NCCR-Mageuzi), alidokeza kusudio la Marekani kukataa kutoa fedha kwa
ajili ya miradi ya MCC, lakini Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo alikanusha taarifa hizo.