Sakata la Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God jijini Dar, Dk. Getrude Rwakatare (pichani) kufunguliwa kesi ya uharibifu wa mali katika Kituo cha Polisi cha Wazo Hill, limechukua sura mpya baada ya faili la kesi hiyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha, huku ikidaiwa kwamba limeibwa.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God jijini Dar, Dk. Getrude Rwakatare.
Kufuatia kudaiwa kuibwa kwa faili hilo lililopewa namba WH/RB/9029/ 2014, UHARIBIFU WA MALI, mlalamikaji, Grayson Justine Mghamba amemwandikia barua mkuu wa upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni akilalamika kwamba anahisi kuna njama zinaendelea ili kumnyima haki yake.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, Kinondoni jijini Dar, zinadai kwamba Grayson alimwandikia barua mkuu huyo wa upelelezi Desemba 2, mwaka huu akiomba msaada kuhusu shitaka hilo aliloripoti polisi Novemba 20, 2014 akimtuhumu mama Rwakatare kumvunjia nyumba yake na kumpora kiwanja kilichopo eneo la Bunju B, Kinondoni.
Sehemu ya barua hiyo ambayo Uwazi inayo nakala yake, inasomeka:
“Nasikitika kusema kuwa kila nifuatiliapo faili langu ili niweze kumjua mpelelezi wa kesi yangu, naambiwa kwamba halionekani wakati wao ndiyo waliniambia nifuatilie.”
Uwazi lilipomtafuta Grayson na kumuuliza kuhusu sakata hilo, alikiri kuandika barua hiyo na kusema kwamba amefuatilia zaidi ya siku tano kwenye Kituo cha Polisi cha Wazo Hill alikofungulia kesi hiyo lakini anaambiwa faili halionekani.
“Nimejaribu kuwaambia kama hilo faili la kwanza limeibwa basi wafungue lingine lakini wamekataa,” alisema Grayson ambaye habari yake ya kuvunjiwa nyumba na mama Rwakatare iliripotiwa kwa mara ya kwanza na Gazeti la Uwazi wiki iliyopita ikiwa na kichwa cha habari: MAMA RWAKATARE AFIKISHWA POLISI.
Katika malalamiko yake, Grayson anadai kuvunjiwa nyumba yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 na mchungaji huyo, ambayo aliijenga kwa fedha alizochukua mkopo kazini kwake.
Grayson alidai kwamba nyumba yake hiyo ilivunjwa na greda kipindi alipoenda Moshi kwenye msiba wa baba yake na kiwanja chake anachodai kukinunua kihalali kwa kuandikishana na aliyemuuzia kwenye Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Bunju B, kuzungushiwa ukuta.
Uwazi lilipomtafuta Mchungaji Rwakatare na kumhoji kuhusu sakata hilo, alisema kwamba kiwanja hicho ni mali yake tangu mwaka 2005 na alivunja nyumba hiyo kwa sababu alikuwa akikifanyia usafi kiwanja hicho alichodai kilivamiwa.