OKTOBA
20 hadi 24 mwaka huu, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliandaa semina kwa
waandishi wa habari, mjini Bagamoyo kujifunza mambo mbalimbali.
Miongoni mwa mada zilizotolewa ni ukweli kuhusu umoja wa fedha katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mada hiyo Ilitolewa na Mchumi Mwandamizi kutoka Idara ya Utafiti BoT,
Dk Suleiman Missango ambaye anaelezea ukweli kuhusu umoja huo.
Miongoni mwa mambo aliyoyatolea ufafanuzi ni maeneo makuu ya itifaki
ya umoja wa fedha, mambo muhimu ya kutekeleza kabla ya kuanzisha umoja
wa fedha, mambo muhimu yatakayotokana na umoja wa fedha, manufaa ya
umoja wa fedha na changamoto.
Umoja wa Fedha
Dk Missango anasema majadiliano ya kuandaa itifaki hiyo yalianza
Januari 2011 na kukamilika Julai, 2013. Kukamilika huku kunatokana na
itifaki hiyo kupitishwa na mkutano wa tatu wa baraza la mawaziri wa
sekta ya umoja wa fedha na kuidhinishwa na mkutano wa dharura wa 27 wa
baraza la mawaziri la jumuiya uliofanyika Julai 2013 na kuridhiwa
na baraza la mawaziri la sekta ya sheria na katiba Novemba 15, 2013.
Anaeleza itifaki hiyo ilisainiwa na wakuu wa nchi wa Jumuiya Novemba
30, 2013. Wakuu wa nchi wanachama waliagiza Itifaki hiyo iridhiwe na
nchi zote wanachama ifikapo Julai, 2014, ili itekelezaji wake uanze mara
moja.
Maeneo makuu ya itifaki ya umoja wa fedha
Akizungumzia itifaki ya umoja wa fedha, Dk Missango anaeleza ina
maeneo makuu 10 ambayo eneo la kwanza linaelezea tafsiri ya maneno
yaliyotumika katika Itifaki.
Eneo la pili linaelezea uanzishaji wa umoja wa fedha, madhumuni yake
na upeo wa ushirikiano katika umoja wa fedha. Katika eneo hili, Itifaki
inaanisha kuwa umoja wa fedha utaanzishwa hatua kwa hatua kwa kuzingatia
mpango kazi ulioandaliwa, na nchi wanachama kufikia vigezo
vilivyokubalika vya muunganiko wa uchumi mpana na masharti mengine
yaliyoanishwa katika Itifaki.
Anasema eneo la tatu linaainisha shughuli muhimu za kukamilishwa na nchi wanachama kabla ya kuingia kwenye umoja wa fedha.
Katika eneo hili nchi wanachama zinakubaliana kukamilisha utekelezaji
wa iItifaki ya umoja wa forodha na itifaki ya soko la pamoja kama
msingi wa kujenga uchumi imara utakaopelekea kuunda umoja wa fedha
tulivu na stahimilivu.
Aidha, nchi wanachama zinakubaliana kurazinisha (hormonise) sera za
bajeti, sera za fedha, na sera za ubadilishaji wa fedha za kigeni, ili
kurahisisha uanzishwaji wa umoja wa fedha na pia kujenga ukanda tulivu
wa kifedha ndani ya Jumuiya.
“Eneo la nne linaainisha vigezo vilivyokubalika vya kupima utayari wa
nchi wanachama kujiunga na umoja wa fedha na utaratibu wa upimaji wa
utekelezaji wake,”anafafanua Dk Missango.
Anasema eneo la tano linaanisha mahusiano katika sera za uchumi mpana
wa nchi wanachama. Katika eneo hili Itifaki inabainisha kuwa jukumu la
kutunga sera ya fedha (monetary policy) na sera ya ubalishanaji wa fedha
za kigeni (exchange rate policy) litakuwa chini ya Benki Kuu ya Jumuiya
na jukumu la kutunga na kutekeleza sera za bajeti (fiscal policies)
litabaki kwa nchi wanachama.
Hata hivyo, ili kuondoa uwezekano wa mgongano wa kisera, nchi
wanachama zitatakiwa kurazinisha na kuratibu utekelezaji wa sera zao za
kibajeti.
Aidha, nchi wanachama zinatakiwa kuzingatia nidhamu ya kibajeti, ili
kutodhoofisha umoja wa fedha na kusababisha mdororo wa uchumi ndani
jumuiya.
“Katika eneo la sita nchi wanachama zinakubaliana kuimarisha na
kuendeleza sekta ya fedha pamoja na kuimarisha na kuunganisha mifumo ya
malipo (Payment and settlements systems), ili kurahisisha muamala wa
kibiashara ndani ya umoja wa fedha,”anaeleza Dk Missango.
Anaeleza eneo la saba linahusu takwimu ambapo nchi wanachama
zinakubaliana kuandaa mfumo wa pamoja wa kuandaa, kuchambua na kutoa
takwimu sahihi kwa ajili ya utekelezaji wa umoja wa fedha.
Anasema katika eneo la nane, nchi wanachama zinakubaliana kuwa na
sarafu moja baada ya kutimiza vigezo vya muunganiko wa uchumi mpana
vilivyokubalika.
Pia kwa kutambua kuwa nchi zote wanachama haziwezi kufikia vigezo
hivyo na masharti mengine ya kuanzisha umoja wa fedha kwa wakati mmoja,
itifaki inaruhusu angalau nchi tatu zikifikia vigezo na masharti
yaliyoanishwa katika Ibara ya 5 na 6 zianze kutumia sarafu moja. Aidha
nchi nyingine zinaweza kujiunga baada ya kutimiza vigezo hivyo.
Anabainisha kuwa eneo la tisa linaainisha taasisi muhimu
zitakazoanzishwa kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa umoja wa fedha.
Taasisi ya kwanza ni Benki Kuu ya Jumuiya (The East African Central
Bank) ambayo kwa kushirikiana na Benki Kuu za nchi wanachama zitaunda
mfumo wa benki kuu wa Jumuiya (EAC system of Central Banks).
Katika mfumo huo, Benki Kuu ya Jumuiya itakuwa na jukumu la kutunga
sera na benki kuu za nchi wanachama zitabaki na jukumu la utekelezaji wa
sera husika (Ibara ya 20).
Taasisi nyingine zitakazoundwa ni pamoja na taasisi ya takwimu,
taasisi ya kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa matakwa ya itifaki ya
umoja wa fedha, ili kuhakikisha kuwa Jumuiya inaunda umoja wa fedha
tulivu, endelevu na stahimilivu, na taasisi mbalimbali za kusimamia na
kuratibu sekta za fedha.
Kwa mujibu wa mkataba wa uanzashaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Wakuu wa nchi wanachama wataunda taasisi zilizotajwa baada ya kupata
mapendekezo kutoka baraza la mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Eneo la kumi na la mwisho linaelezea kuhusu masuala ya ujumla
ikiwemo Itifaki kupata nguvu ya kisheria baada ya kuridhiwa na nchi zote
wanachama,”anaeleza Dk Missango.