KATIKA kutatua baadhi ya changamoto zinazohusu masuala ya elimu
kwa vijana nchini, imebainika hali hiyo wakati mwingine inachangiwa na
sekta husika kutokuwa na mawasiliano ya karibu.
Hata hivyo, baadhi ya wadau baada ya kubaini changamoto hizo hivi
sasa wanajipanga kujenga mtandao katika sekta zote za elimu na kuwa
kitu kimoja.
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugezi Mkuu wa Global Education Link LTD
(Gel), Abdulmalik Mollel, anasema ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu
changamoto hizi wameandaa maeonyesho ya elimu.
Maonyesho hayo ya kwanza na kimataifa ambayo yanatarajiwa kufanyika
katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, kuanzia Desemba 10 hadi 14
mwaka huu.
Anasema maonyesho hayo yanaandaliwa na kuratibiwa na Global Education
Link Ltd (Gel), kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi),
Wizara ya Elimu, Mafunzo na Ufundi na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara
Tanzania (TanTrade).
“Maonyesho haya yanatarajiwa kuvuta washiriki zaidi 500 na watembeleaji zaidi ya 350,000 kutoka ndani na nje ya nchi.
“Kaulimbiu ya maonyesho haya ni ‘Kuweka jitihada za pamoja katika
kuboresha mfumo wa elimu Tanzania ni njia thabiti ya kuleta maendeleo
endelevu katika taifa,” anasema Mollel.
Mollel anasema lengo kuu la maonyesho hayo ni kuwaunganisha wadau
wote wa elimu kwa pamoja, ili waweza kutoa huduma kwa wananchi na
kuwaelimisha juu ya mambo muhimu yaliyopo katika sekta husika.
Anafafanua kwa kuwataja wadau wa sekta binafsi wa elimu ambao ni
mifuko ya pensheni, wachapishaji wa vifaa vya shule, taasisi za
kielimu.
Nyingine ni asasi za kielimu, vyuo vikuu vya elimu vya ndani na nje
ya nchi, shule za awali na sekondari pamoja na wadau wengine,
akibainisha kuwa itakuwa ni sehemu yao kuuza bidhaa zao mbele ya wadau
lengwa.
Mollel anasema maonyesho hayo yataleta manufaa makubwa na changamoto
chanya hasa kuongeza ushindani katika sekta ya elimu ambayo itasaidia
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (RBN).
“Warsha kama hizi za elimu zina lengo la kuhamasisha ubora wa elimu
na uchumi kutokana na hali halisi ya nchi yetu,”anasema Mollel.
Anataja baadhi ya faida katika ushiriki wa asasi mbalimbali nchini
kwa uchache ni pamoja na kutengeneza ushindani wa bidhaa za elimu
katika sekta za elimu nchini zitakazosababisha elimu yenye tija na
kwenda na soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Faida nyingine ni njia pekee ya kubadilishana na kuonyeshana ujuzi
kutoka shule moja hadi nyingine, na wananchi watapata fursa ya kupata
nafasi ya shule au chuo na kuweza kupata taarifa kwa uwazi juu ya elimu
ya ndani katika eneo moja bila urasimu ndani ya eneo husika.
Pia wananchi watapata nafasi ya kuchagua kozi na kuzielewa vizuri
kabla ya kufanya maamuzi yao ya mwisho na wanafunzi wazazi watapata
ushauri kuhusu kozi mbalimbali wanazotaka watoto wao wakasome.
“Tume ya Vyuo Vikuu, sekta mbalimbali za elimu, benki na washiriki
wengine toka nje ya nchi zitapata nafasi ya kutoa mada na kuuza
biashara zao kwa wananchi zinazohusiana na bidhaa za elimu,”anaeleza
Mollel.
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Jacqueline Maleko, anasema ili kuweza
kufanya vizuri katika mambo mbalimbali yanayohusu biashara ni lazima
kuwa na elimu ya kutosha, hivyo maonyesho hayo yatawasaidia wanafunzi
kupata elimu bora itakayowasaidia kufanya biashara zao kwa umakini.
“Kama sekta ya elimu hatutaijengea mazingira mazuri na vijana
wakaweza kujiari, kuna hatari hapo baadaye nchi ikaja kuingia katika
mifarakano makubwa.
“Wakati vijana wa mataifa ya wenzetu walipata nafasi mbalimbali za
kazi hapa nchini wa kwetu wanakosa kwa madai kuwa hawaajiriki,”anasema
Jacqueline.
Anasema vijana wengi wa nje wanapata ajira nchini kwa sababu nchi zao
zimekuwa zikifanya vizuri katika kujitangaza kimataifa.
“Sisi tunavyo vyuo vikuu ambavyo ni vizuri, lakini tunashindwa kuvitangaza," anasema Jacqueline.
Hata hivyo, Maleko amewataka wanafunzi pamoja na wazazi kujitokeza kwa wingi katika maonyesho.