SIKU
moja baada ya Jeshi la Polisi kudhibiti maandamano yaliyoandaliwa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wafuasi watatu wa chama
hicho wamefikishwa mahakamani jijini Dar es Salaam na wengine watano
wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro.
Wafuasi hao watano wa mkoani Morogoro wanashikiliwa na polisi wakidaiwa
kupinga agizo lilitolewa na viongozi wa jeshi hilo la kuwataka
kutoandamana.
Wanachama waliokamatwa ni pamoja na Witnes Makoyola (29), Katibu wa
Chadema tawi la Kiwanja cha ndege, Shukuru Makamba(46), Maria Lissu (28)
mkazi wa Kilakala na Katibu wa Baraza la Wanawake wilaya ya Morogoro
Mjini, Hussein Hassani (28) mkazi wa Mafiga na Odwin Peter (65) mkazi wa
Kiwanja cha ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani
Morogoro, Leonard Paul alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa
5:30 asubuhi katika maeneo ya mtaa wa Konga.
Kamanda Paul alisema Septemba 17 viongozi wa chama hicho waliandika
barua ya kuomba kuandamana, huku wakidai kuwa lengo la maandamano hayo
ni kupinga hatua ya wabunge wa Bunge la Katiba kuendelea na vikao huku
wakijua kuwa katiba haitapatikana.
Aidha Kamanda Paul alisema kuwa barua hizo zilienda kwa wakuu wa polisi
na kwamba jeshi hilo lilizuia maandamano kutokana na taarifa za
kiintelijensia kuwa wapo baadhi ya wananchi walipanga kufanya uhalifu
wakati wa maandamano, ikiwa ni pamoja na kuwa kesi ya suala hilo bado
iko mahakamani.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema kuwa jeshi hilo liliwaita viongozi wa
chama hicho, lengo likiwa ni kuwazuia kuandamana ambapo alisema kuwa
jana majira ya saa 5:30 asubuhi katika maeneo ya mtaa wa Konga kulianza
kufanyika mkusanyiko wa watu wakijiandaa kuandamana baada ya kuweka
ulinzi katika maeneo yote waliyopanga kuanzia maandamano ya wafuasi wa
chama hicho.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema walifanikiwa kutawanya mkusanyiko huo
kwa kurusha mabomu ya machozi sambamba na kuwakamata watuhumiwa hao
ambapo alisema kuwa watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.
Kwa upande wake katibu wa chama hicho mkoani hapa, Boniface Ngonyani
alisema kuwa maandamano hayo yaliyotarajiwa kufanyika jana majira ya saa
5.00 asubuhi yalizuiwa na jeshi la polisi ambapo jeshi hilo lilidaiwa
kuingia ndani ya ofisi za chama hicho na kuanza kupekua nyaraka na
kuzitwaa nyingine na kuondoka nazo.
Aidha alisema baada ya hekaheka hiyo baadae wakabaini kwamba kompyuta
mpakato ya Mwenyekiti wa Chadema Wilaya, James Mkude pamoja na simu yake
ya mkononi havionekani.
Hata hivyo, alisema kutokana na kukamatwa kwa wanachama hao ofisi ya
Chadema mkoa wa Morogoro tayari imewatuma wanasheria wake wawili ili
kuweza kufika polisi na kuangalia tatizo lililofanya kukamatwa kwa
wanachama hao.
Na habari kutoka mkoani Dar es Salaam, wafuasi watatu wa Chadema
wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuingia katika Makao Makuu ya
Jeshi la Polisi kinyume na utaratibu.
Wafuasi hao ambao walifikishwa mahakamani hapo jana ni Ngaiza Kamugisha
(28) dereva, mkazi wa Vingunguti, Benito Mwapinga (30) Fundi nguo mkazi
wa Mtoni kwa Azzi Ally na Eliasante Bugeji (51) Mhasibu wa Hospitali ya
CCBRT mkazi wa Komakoma Kinondoni, Dar es Salaam.
Akisoma hati ya mashitaka Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola
akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka na George
Barasa, ambapo alidai kuwa wafuasi hao wanakabiliwa na mashtaka matatu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Kongola alidai mashtaka hayo ni kuingia kwa nguvu Makao Makuu ya Jeshi
la Polisi, kukaidi amri halali na kutoa lugha ya matusi.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Septemba 18 mwaka huu, washtakiwa
waliingia kinyume cha sheria ndani ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa
hali ya fujo.
Aidha, ilidaiwa katika tarehe hiyo na maeneo hayo washtakiwa walikataa
kutii amri ya halali ya kutawanyika kutoka eneo la makao hayo ya polisi
iliyotolewa na Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Inspekta Zuhura, ambaye
alitoa amri hiyo baada ya kuruhusiwa na viongozi wake.
Akiendelea kusoma mashitaka hayo, alidai katika kosa la tatu linamkabili
Bugeji peke yake, inadaiwa akiwa katika mazingira ya Makao Makuu ya
Jeshi la Polisi alitoa lugha ya matusi kwa maofisa wa Polisi. Ilidaiwa
maneno hayo yaliyotolewa na mshitakiwa huyo yalikuwa yakiashiria
uvunjivu wa amani.
Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na upande wa mashitaka umeomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Wakili wa wafuasi hao Peter Kibatala alidai mashtaka yanayowakabili
washtakiwa yanadhaminika, hivyo akaomba mahakama iwapatie masharti nafuu
kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Kongola aliendelea kudai kuwa mahakama inatakiwa itoe
masharti yanayoendana na mazingira ambayo washtakiwa wametenda kosa
hilo. Kibatala alidai kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania dhamana ya washtakiwa ni haki yao na pia washtakiwa bado
haijawatia hatiani, kwa hiyo dhamana ni haki yao.
Hakimu
Moshi alisema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana wanatakiwa wawe na
wadhamini wawili wa kuaminika wakiwemo watumishi wa Serikali au
watumishi kutoka katika Taasisi inayotambulika wakiwa na barua za
waajili wao na vitambulisho vya kazi na wadhamini watasaini bondi ya Sh
500,000 kwa kila mmoja.
Kesi
hiyo iliahirishwa hadi Septemba 24 mwaka huu kwa washtakiwa kusomewa
maelezo ya awali na akaamuru washtakiwa warudishwe rumande kwa sababu
hawakuwa na wadhamini.
Mpaka gazeti hili linaondoka katika eneo la Mahakama washtakiwa walikuwa
hawajapata dhamana, ambapo kulikuwa na jitihada za kupiga simu Makao
Makuu ya Chadema ili wapate wadhamini.
Nje ya mahakama Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Nickson Tugala
alikuwa aking'ang'ania kuingia mahabusu kuwaona washtakiwa, jambo ambalo
lilisababisha fujo katika eneo hilo. Tugala alionekana kubishana na
Insepkta wa Jeshi la Polisi, Mussa Mkini mpaka kufikia hatua ya
kusogelea kwa karibu hali iliyowatia hofu watu waliyokuwa katika eneo
hilo kuwa watu hao wanataka kupigana.
Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Mkini aombe nguvu kutoka Polisi na
ilipofika saa 6:10 mchana ziliingia gari mbili za polisi namba PT 1846
na PT 1145 zikiwa na askari wenye silaha za moto. Mkini alitoa amri ya
Tugala kuchukuliwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Mkoa wa Dar
es Salaam kutokana na fujo ambazo alikuwa anafanya, lakini bado Tugala
alikuwa akiwagomea askari hao.
Baadaye alikubali kuondoka nao, ambapo askari wawili walipanda kwenye
gari ambalo alikuwa akiendesha la M4C namba T 351 CAY. Askari mmoja
alipanda ndani ya gari na mwingine alipanda nyuma ya gari hilo
wakiongoza kwenda Central.
Chanzo:Habarileo