Rais Jakaya Kikwete.PICHA|MAKTABA
Jeshi la Polisi mkoani Tanga juzi lilisema kwamba kuna zaidi ya bandari
bubu 50 katika mkoa huo ambazo zinaingiza bidhaa ambazo hazilipiwi
ushuru, huku nyingine zikiwa bandia.
Laiti Rais Jakaya Kikwete angekuwa na utaratibu
wa Serikali yake kufanya tathmini endelevu ya utekelezaji wa kazi wa
mawaziri katika wizara zote, angegundua kwamba zipo baadhi ya wizara
ambazo viongozi wake ni mizigo isiyobebeka kutokana na kutofanya kazi,
huku wakilipwa mishahara minono. Mfano hai ni Wizara ya Viwanda na
Biashara, ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa ikilalamikiwa na wananchi
kwa kutotimiza majukumu yake. Ni wizara ambayo wananchi wengi wanasema
haina lolote la kujivunia, kinyume na baadhi ya wizara, ambazo utendaji
kazi wa mawaziri wake siyo tu umetukuka, bali pia ni wa kutolea mfano.
Wakati wa kuzindua mpango wa Serikali wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) miezi kadhaa iliyopita, tuliambiwa kwamba mawaziri
wote walipewa malengo ya utekelezaji wa mpango huo na kwamba kila waziri
alisaini mkataba maalumu mbele ya Rais Kikwete, ‘akila kiapo’
kutekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa mkataba huo. Vinginevyo
angewajibishwa, kwa maana ya kupoteza kazi yake. Wapo mawaziri ambao
wameonyesha uwajibikaji mkubwa katika utekelezaji wa malengo
yaliyowekwa, lakini pia wapo mawaziri ambao wameendelea kufanya kazi kwa
mazoea.
Pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili Wizara
ya Viwanda na Biashara, wananchi hawaoni nini kinafanyika katika
kukabili changamoto hizo. Jana katika safu hii tulizungumzia changamoto
ya ukosefu wa masoko kwa mazao ya biashara na chakula, tukisema wakulima
wameachwa njia panda kwa mazao yao kutonunuliwa, huku wakibakia katika
umaskini uliopitiliza.
Tunapozungumzia masoko tuna maana ya masoko ya
ndani na nje ya nchi. Tani zaidi ya 16 milioni za mahindi ya wakulima
zilizorundikana katika mikoa ya Morogoro, Rukwa, Katavi, Mbeya na Iringa
kwa kukosa soko ni ushahidi usioacha shaka kwamba wizara inayohusika na
biashara haina mbinu na mikakati ya kumaliza kero hiyo.
Ni kazi ya wizara hiyo kwa kushirikiana na wizara
inayohusika na uwezeshaji kuwaunganisha wakulima na mitandao ya masoko
mbalimbali. Sukari inayozalishwa nchini imelundikana katika maghala kwa
kukosa soko, huku bidhaa hiyo kutoka nje ikiingizwa nchini kwa bei ndogo
kwa sababu ya kutolipiwa kodi. Wizara hiyo haijui kinachoendelea,
ingawa inazo habari kwamba bidhaa nyingi zisizolipiwa ushuru zinaingizwa
nchini kupitia bandari nyingi bubu zilizoenea katika maeneo ya Pwani ya
Bahari ya Hindi, yakiwamo maeneo ya Mbweni, Mlingotini, Ununio, Kawe,
Msasani, Kunduchi, Kigamboni, Tegeta na Bagamoyo.
Tatizo la kuwapo bandari bubu linazidi kuongezeka.
Jeshi la Polisi mkoani Tanga juzi lilisema kwamba kuna zaidi ya bandari
bubu 50 katika mkoa huo ambazo zinaingiza bidhaa ambazo hazilipiwi
ushuru, huku nyingine zikiwa bandia. Itakumbukwa kuwa, Waziri wa
Biashara na Viwanda, Abdallah Kigoda alisema bungeni mwaka 2013 kuhusu
kuwapo kwa bandari bubu na upitishaji wa bidhaa bandia katika maeneo
mengi nchini. Kwa nini wizara husika haichukui hatua ni swali ambalo
pengine linaweza kujibiwa na waziri huyo pekee.
Ndiyo maana wananchi wengi wanasema wizara hiyo ni
mzigo, kwani imeshindwa siyo tu kuendeleza viwanda vidogovidogo, bali
pia kuanzisha viwanda vya kusindika matunda kama nanasi, nyanya, maembe
na machungwa ili wakulima wapate masoko ya mazao hayo. Ni kwa sababu
hiyo tunasema wizara hiyo inahitaji waziri na watendaji wenye ubunifu na
moyo wa kuwatumikia wananchi.