Klabu ya Yanga imemleta nchini
kwa majaribio mshambuliaji raia wa Zambia, Jonas Sakuwaha anayeichezea
klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Sakuwaha (31), pia amewahi kucheza soka katika
klabu ya Zesco United (Zambia), Lorient (Ufaransa), Le Havre (Ufaransa)
na El-Merreikh (Sudan).
Kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa Yanga, kama
Sakuwaha atafuzu majaribio, basi atachukua nafasi ya Hamis Kiiza raia wa
Uganda katika orodha ya wachezaji wake watano wa kigeni kwa mujibu wa
kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mbali na Kiiza, Haruna Niyonzima yuko hatarini
kuiacha Yanga na tayari Azam FC imemkaribisha kundini ikijinasibu kuwa
raia huyo wa Rwanda ni mchezaji wao.
Azam wamekuwa wakidai kuwa walikuwa wa kwanza
kumsajili Niyonzima kabla ya kutua Yanga, lakini aliyekuwa kocha wao,
Stewart Hall alimkataa kwa kigezo cha ufupi, ndipo walipomshauri ajiunge
na Yanga.
Yanga tayari inao wachezaji watano wa kigeni ambao
ni, Mbuyu Twite, Andrey Coutinho, Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima na
Mbrazili mpya, Emerson de Oliveira Neves Rouqe, anayetarajiwa kuwasili
nchini kesho kuziba nafasi ya Mbrazili Genilson Santos ‘Jaja’.
Kuwasili kwa Sakuwaha aliyeichezea Zambia michuano
mbalimbali ya kimataifa na pengine ujio wa Emerson ni mabadiliko
yanayolenga kuimarisha mfumo wa uchezaji Yanga.
Hata hivyo, hilo litategemea kuondoka kwa Kiiza na Niyonzima, ambao wameonyesha nia ya kutotaka kubakia kwenye klabu hiyo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza
kuwa Sakuwaha atawasili nchini akifuatana na wachezaji wengine wanne
kutoka Zambia kwa ajili ya majaribio.
Jana kulikuwa na habari kuwa mshambuliaji chipukizi wa Uganda, Yunus Sentamu anayeichezea AS Vita ya DRC, naye atatua Yanga.
Katika hatua nyingine, Emerson de Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili nchini kesho saa 7.00 mchana kwa ajili ya majaribio.